Nchemba, Msigwa nusura
wazichape Dodoma
Dodoma. Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba jana nusura wachapane makonde baada ya kutupiana maneno ya kashfa, wakituhumiana kuhusika na mlipuko wa bomu uliotokea Jumamosi iliyopita mkoani Arusha.
Tukio hilo lilitokea katika viwanja vya Hoteli ya St Gasper nje
kidogo ya mji wa Dodoma, walipokwenda kwa ajili ya kuhudhuria semina ya
wabunge wapambanaji na Ukimwi, ambapo baadhi ya wabunge wa Chadema
walihudhuria, baada ya kutoonekana mjini humo tangu Juni 17 mwaka huu.
Wabunge hao wa Chadema hawakuhudhuria kikao chochote cha Bunge
kutokana na kwenda mkoani Arusha kwa shughuli mbalimbali, kutokana na
mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wao wa kuhitimisha kampeni zake
za uchaguzi mdogo wa udiwani katika viwanja vya Soweto, Juni 16 jijini
humo.
Malumbano hayo yanatokana na Nchemba kuituhumu Chadema kuhusika na
mlipuko huo, Juni 20 mwaka huu wakati akichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya
Serikali ya mwaka 2013/2014, akisema chama hicho kilipanga kulipua bomu
hilo ili kuwafanya Watanzania waamini kuwa Serikali ya CCM ndiyo
inayohusika na tukio hilo.
Ilivyotokea
Wakati Msigwa akiingia katika ukumbi huo akiwa ameongozana na Mbunge
wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje, walikutana uso kwa uso na Nchemba
ambaye alikuwa akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Amour
Arfi.
Baada ya Nchemba kumwona Msigwa alimkaribisha mchungaji huyo akisema; “Karibu sana bwana, salama lakini?”
Hata hivyo, badala ya kujibu salamu hiyo ya Nchemba, Msigwa alikuja
juu na kumtuhumu Nchemba kwamba anatoa kauli zinazoweza kuvuruga amani
ya nchi.
“Wewe ni mtu hatari sana, haya yote yanasababishwa na wewe, mnatumia
damu za watu kutafuta madaraka,” alisema Msigwa akimtupia maneno
Mwigulu.
Baada ya kauli hiyo Nchemba alihoji akisema: “Ki-vipi? Hayo mambo tuyaache, Msigwa achana na haya mambo!”
Baada ya Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM kujibu,
Msigwa alimsogelea karibu na kumnyooshea kidole, huku akiendelea
kumtuhumu kuwa ana siasa chafu zinazopandikiza chuki kwa jamii.
Malumbano hayo pia yaliingiliwa na Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema),
Vicent Nyerere ambaye alimuunga mkono Msigwa, huku akimtuhumu Nchemba
kuwa ni mtu mbaya katika siasa za Tanzania. Katika kile kilichoonekana
kutaka kuweka mambo sawa, Wenje alimvuta Msigwa na kumpeleka ukumbini
ili kuepusha shari baada ya wabunge hao kuzidi kurushiana maneno.Hata walipoingia ndani ya ukumbi huo wabunge hao waliendelea kulumbana, lakini wakatulizwa na baadhi ya wabunge waliokuwa karibu yao.
Alipotakiwa kueleza sababu za mzozo huo na Nchemba, Mchungaji Msigwa
alisema, “Achana na yule mpuuzi, mimi siwezi kuzungumza na mtu mnafiki,
mkatili na yeye ndiye alihusika na mipango mibaya dhidi ya Chadema hata
mlipuko wa Arusha hivyo kutesa watu wa Chadema.”
Alisema kuwa yeye haoni sababu ya mtu mwenye mipango mibaya na
wananchi wa Tanzania pamoja na chama chake (Chadema), kuwafuata na
kujikomba.
Kwa upande wake Nchemba alipoulizwa alisema kuwa alichokizungumza ni
mtazamo wake na kwamba ikiwa kuna mtu anayeona kuwa alizungumza uzushi,
ajitokeze na kupinga. “Nilichokizungumza ndicho kilichofanyika kwa
matukio yote niliyoeleza bungeni,”alisisitiza Nchemba.
Alichokisema bungeni
Wakati akichangia mjadala wa Bajeti, Nchemba alisema hata ripoti
iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri baada ya kutekwa kwa Mwenyekiti wa
Jukwaa hilo, Absalom Kibanda, ilieleza kuwa watu waliohojiwa walidai
kuwa Chadema kimepewa mafunzo kutoka nje ya nchi, kwamba kikitumia
baadhi ya viongozi wa dola wasiokuwa waaminifu kuteka watu na hata kuua
watu maarufu, watu wataamini CCM imeshindwa kuongoza nchi na sasa
imeanza kuua watu.
Akizungumzia mkanda wa video unaoonyesha tukio la mlipuko wa bomu la
Arusha, Nchemba alisema kuwa tukio hilo lilipangwa na ndiyo maana
Chadema walipanga hadi wakarekodi tukio hilo.
“Lile tukio limepangwa na ndiyo maana hata aliyechukua ile video
hakustushwa kabisa na mlipuko wa bomu, jambo hilo haliwezekani kabisa,
tukio lile limepangwa kwa kiwango cha chini kabisa,” alisema na
kuongeza; “Mtu yule alikuwa akichukua video utadhani yuko katika harusi,
CCM haijashiriki katika tukio la Arusha, ila kutokana na nguvu ya chama hiki ni lazima kitahusishwa na tukio hilo.”