Elikana, Eliud; Watoto walioungana wanaotumia njia moja kujisaidia
“Madaktari waliponiambia kuwa watoto
wangu wameungana nilichanganyikiwa, niliona dunia imenigeuka, sikuwahi kuwaza
nitakutana na kitu cha namna hii katika maisha yangu.”
Ni maneno ya binti
kutoka Mbeya, Grace Joel (19), ambaye Februari 20 mwaka huu, alijifungua pacha
wa kiume ambao wameungana katika sehemu ya kiunoni.
Mwanadada huyo
anasema hakuamini macho yake pale madaktari wa Hospitali ya Uyole iliyopo
mkoani humo walipomwambia kuwa watoto wake wameungana na hivyo kupewa rufaa ya
kwenda kwenye Hospitali Kuu ya Mkoa wa Mbeya.
“Wakati wa ujauzito wangu sikuwahi hata
siku moja kuhisi kuwa ningeweza kuzaa watoto wakiwa kwenye tatizo hili,
sikuwahi kuumwa zaidi ya kuvimba miguu tu na hiyo ni hali ya kawaida kwa
mjamzito yeyote.” anasema Grace ambaye kwa sasa
anahitaji msaada wa hali na mali ili kuokoa maisha ya watoto wake.
Licha ya umri huo
mdogo, amejikuta kwenye hali ya mateso na uchungu mwingi baada ya familia yake,
hususani mume wake, Erick Mwakyusa kumtelekeza kwa kile alichodai kuwa hana
haja na watoto walioungana.
“Nilishangaa, familia yangu kunitelekeza
katika hali hii baada ya kugundua watoto wameungana, mume na familia yake
alinitamkia wazi kuwa hawana shida na watoto walioungana, alisema hawezi
kuwalea kwa kuwa kwao hakuna watoto wenye ulemavu wa aina hiyo,”
anasema.
“Siyo siri nilijisikia uchungu,
sikuamini kuwa mume wangu angenifanyia hivyo, siyo yeye tu hata familia yao
yote sikudhani kama wangenigeuka hivyo, nashukuru kwa upande wa familia ya
wazazi wangu walikuwa pamoja nami ingawa ni maskini na hawana uwezo wa
kunisaidia.
“Hospitali ya Kyela ndiyo iliyonipeleka
ile ya Rufaa Mbeya ambao nao walivyoona hali ya watoto wangu wakanishauri kuja
Muhimbili, sikuwa na uwezo wa kufika hapa, lakini nawashukuru madaktari wa
Rufaa Mbeya walioniwezesha kufika hapa.
Grace anasema watoto
wake hao, Elikana na Eliud aliwazaa wakiwa na uzito kilo tano na nusu na
walifika Hospitali ya Taifa Muhimbili wiki mbili tangu kuzaliwa kwao.
Wanatumia njia moja
kujisaidia
Dk Zaituni Bokhari,
ambaye ni Daktari Bingwa katika Kitengo cha Upasuaji kilichopo Hospitali ya
Taifa Muhimbili, anasema kutokana na namna walivyoungana, wanatumia njia moja
kujisaidia.
“Njia ya kukojolea wanatumia moja na pia
njia ya haja kubwa wanatumia moja, tutakapowatenganisha kuna utaalam ambao
utafanywa ili kila mtu aweze kutumia njia yake mwenyewe bila athari zozote,”
anasema.
Anaeleza
kwamba, iwapo upasuaji huo utafanikiwa watoto hao watakuwa kule India kwa wiki
mbili ndipo watarejea nchini na kuendelea na matibabu chini ya uangalizi wa
wataalamu wa Hospitali ya Muhimbili hadi pale afya zao zitakapoimarika.Kutokana na hali ya kiuchumi ya mama huyo, Dk. Bokhari amewataka wasamaria wema kujitokeza na kutoa misaada mbalimbali kama ya maziwa, nguo na fedha kwa ajili ya vitu vidogo vidogo ili aweze kuwahudumia vyema watoto wake.
Dk. Bokhari anasema wao waliwapokea watoto hao wakiwa katika hali mbaya kutokana na uchovu wa safari kwa basi kutoka Mbeya na walikuwa na maambukizi sehemu mbalimbali.
“Walikuwa ni wachanga kabisa, walikuwa na wiki mbili, walikuwa wamechoka kutokana na mwendo mrefu wa basi kutoka Mbeya, walikuwa na homa kali na matatizo katika njia ya kupumua, tukatibu kwanza matatizo hayo ndiyo vipimo vingine vikaendelea,” anasema.
“Wamefika hapa hawakuwa hata na nguo za kutosha, huyu mama naye alikuja katika hali ya kuchanganyikiwa ukizingatia ukweli kuwa ndugu zake wamemtelekeza, tumefanya kazi kubwa sana ya kumpa ushauri nasaha mpaka akakubaliana na hali halisi.
“Kuna wakati alikuwa anasema anataka kuondoka awaache watoto kwetu, hali hiyo ilitokana na kuchanganyikiwa, muda mwingi alikuwa akilia ila kwa sasa namshukuru Mungu yeye na watoto wanaendelea vizuri,” anasema.
Kwa nini wameungana
Dk Bokhari anasema hali ya watoto kuungana siyo ya kurithi kama yalivyo kwa baadhi ya magonjwa.
“Hali hii inaweza kusababishwa na upungufu wa madini,” anaeleza.
Mtaalamu mwingine wa afya ameliambia gazeti hili kuwa, “Pacha wanaofanana kwa kawaida hutokana na yai lililopandikizwa kujigawa mara mbili, baada ya siku 12 mgawanyiko wa seli (chembe chembe) unakuwa umeanza kujipanga kwa ajili ya kujiachanisha katika uumbwaji wa viungo au ogani mbali mbali za mwili”.
Anasema kuwa, jinsi siku zinavyozidi kusogea mgawanyiko wa mapacha kujiachanisha na kujitegemea ikitokea kabla ya seli kufikia wakati wa kuruhusu jambo hilo, ngozi nyembamba za mapacha hao huendelea kuungana na kushikamana.
“Hata hivyo kwa sayansi ya tiba chanzo kikuu hasa hakijulikani,” anaeleza mtaalam huyo.
Matibabu ni India pekee?
Dk Bokhari anasema kutokana na aina ya upasuaji wa watoto hao, inabidi ufanyike kwenye nchi zenye watalaamu na vifaa vya kisasa kama India au Afrika Kusini.
“Upasuaji huu unatakiwa ufanywe na madaktari zaidi ya saba na kila daktari atakabiliana na kiungo chake, mimi pia ni miongoni mwa madaktari ambao nitashiriki upasuaki wa watoto hawa na inatakiwa umakini wa hali ya juu,” anasema.
Anaeleza kuwa, upasuaji wa aina hiyo unaweza kufanyika kwa saa 24 ama chini ya hapo.
No comments:
Post a Comment