|
WATOTO WAKUMBUKWE KIMICHEZO |
>Viwanja vya michezo na sehemu za wazi ni huduma muhimu kwa jamii sehemu mbalimbali duniani.
Kwa muda mrefu jamii ya watu wa Tanzania imekuwa ikishiriki katika michezo mbalimbali katika makabila tofauti.
Kwa mfano kabla ya kuja wakoloni nchini,
Watanzania walikuwa wakishiriki michezo mbalimbali katika makabila yao
kama kucheza mieleka, kutupa mkuki, kulenga shabaha kwa upinde na
mishale, sarakasi, kukimbia, kuruka, kuogelea na kucheza bao.
Walipokuja wakoloni walituletea michezo ya kigeni
kama soka, netiboli, ngumi, hoki, mpira wa kikapu, mpira wa wavu,
tenisi, mpira wa meza, mpira wa mikono, kriketi, gofu, baiskeli na
mingine mingi.
Ujio wa michezo hiyo ya kigeni nchini uliendana na
ujenzi wa viwanja vya michezo hiyo na pia baada ya nchi yetu kupata
uhuru Serikali ya awamu ya kwanza iliendelea kujenga viwanja vya michezo
hiyo.
Serikali ya awamu ya kwanza iliendeleza viwanja na
michezo hiyo ya kigeni kwa kuwa ilitambua michezo ni sehemu ya uhai na
utashi wa taifa letu.
Ndiyo maana Tanzania ilipata mafanikio makubwa
katika michezo kama soka, riadha, ndondi, netiboli na michezo mingine
hasa katika awamu ya kwanza.
Tunasema hivyo kwa sababu tunafahamu Tanzania
ilipata nafasi ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika katika
soka kwa mara ya kwanza wakati Serikali ya awamu ya kwanza ikiwa
madarakani.
Pia, Tanzania inajivunia kupata medali mbili tu za
Olimpiki ambazo zote zilipatikana wakati wa utawala wa Serikali ya
awamu ya kwanza.
Tunafahamu kwamba wakati wa utawala wa Serikali ya
awamu ya pili ndipo viwanja vingi vya michezo vilibadilishwa matumizi
yake, pia maeneo mengi ya wazi yalivamiwa. Hali hiyo iliendelea katika
utawala wa Serikali ya awamu ya tatu na inaendelea mpaka katika utawala
huu wa Serikali ya awamu ya nne.
Tunasikitika kuona Serikali imelifumbia macho
tatizo la viwanja vya michezo nchini kuvamiwa na kubadilishwa matumizi
yake, pia tunasikitika kuona Serikali haijengi viwanja mbalimbali vya
michezo nchini.
Vilevile tunasikitishwa na Serikali kushindwa
kuwazuia watu mbalimbali wasivamie maeneo ya wazi yaliyokuwa yametengwa
kwa ajili ya watoto kuyatumia kwa michezo au watu kupumzika.
Tunashangaa kuona viongozi wa Serikali za mitaa, halmashauri na
manispaa nchini wanashindwa kuelewa kuna ardhi ya biashara na ardhi ya
jamii, lakini wamekuwa wakishindwa kusimamia ardhi ya jamii ambayo
imekuwa ikichukuliwa kwa matumizi ya biashara au matumizi ya watu
binafsi.
Kutokana na ardhi ya jamii kuvamiwa, Tanzania
imekuwa na tatizo kubwa la viwanja vya michezo, maeneo ya wazi na maeneo
ya kupumzika, hivyo kusababisha kukosa wanamichezo mahiri, vijana
kukosa sehemu za kupumzika na hivyo kukimbilia kwenye baa na kumbi
mbalimbali za starehe kwa ajili ya kupumzika.
Tunatarajia kuona Serikali na wizara zote
zinazohusika na usimamizi wa ardhi ya jamii kuhakikisha ardhi ya jamii
haivamiwi na watu wote waliovamia katika ardhi hiyo wanaondolewa.
Tunaamini ardhi ya jamii ni muhimu katika
maendeleo ya jamii kwa sababu ardhi ya jamii inakuwa na viwanja vya
michezo, maeneo ya wazi, viwanja vya kupumzika, ambapo watu huweza
kukutana na kubadilishana mawazo huku, pia watu watafanya mazoezi na
kuepuka maradhi mbalimbali ya mwili na kiakili......