HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. EMMANUEL J. NCHIMBI (MB) WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
KATIKA
SHEREHE YA KUFUNGA MAFUNZO YA UONGOZI NGAZI YAJUU YA MAAFISA WA JESHI
LA MAGEREZA TANZANIA BARA NA VYUO VYA MAFUNZO ZANZIBAR
TAREHE 12 JUNI, 2013
- · Kamishna Jenerali wa Magereza,
- · Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar,
- · Makamishna,
- · Maafisa Waandamizi wa Magereza ,
- · Mkuu wa Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga,
- · Maafisa wa Majeshi mbalimbali,
- · Maofisa na Askari Magereza,
- · Wahitimu,
- · Wageni waalikwa,
- · Wanahabari,
- · Mabibi na Mabwana.
Napenda
nianze kwa kutumia fursa hii kukushukuru sana Kamishna Jenerali wa
Magereza na Uongozi mzima wa Jeshi la Magereza kwa kunialika katika
hafla hii. Ninatoa shukrani hizi kwa kuwa hakuna sheria wala kanuni
inayowalazimisha kunialika kwa hiyo mngeweza kumualika mtu yeyote kuja
kufunga mafunzo haya.
Msingi
huo huo uwepo wangu hapa unanipa fursa ya kukutana na nanyi kwa karibu
na pia unanipa fursa ya kuwakumbusha mambo muhimu ya Kitaifa hasa
matarajio ya Serikali na wananchi kwa Jeshi la Magereza.
Napenda pia kukupongeza Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar kwa kuendelea kuleta Maafisa wako katika Chuo hiki kujifunza taaluma mbalimbali za urekebishaji Wafungwa. Nimefahamishwa
kuwa hii siyo mara ya kwanza kuleta Maafisa kwenye mafunzo kama haya,
nashauri ushirikiano huu uendelezwe kwa maslahi ya amani na usalama
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, nawapongeza sana wahitimu wote wa mafunzo haya kwa kufanya vizuri katika na kustahili kupandishwa vyeo kuwa Warakibu Wasaidizi wa Magereza. Ninatambua
kwamba kupandishwa kwenu cheo ni ishara ya kwamba sasa mmebobea katika
mbinu, maarifa na ujuzi zaidi wa kumudu majukumu yenu. Aidha,
gwaride lenu zuri lenye ukakamavu mkubwa limetudhihirishia namna
mtakavyoenda kutekeleza majukumu yenu mapya kwa ustadi na weledi mkubwa.
Mafunzo katika taasisi yoyote ni sehemu muhimu katika kuleta ufanisi wa
taasisi husika. Hivyo
tunaamini kwamba mafunzo haya waliyoyapata wahitimu wa leo, yataleta
ufanisi mkubwa katika utendaji kazi wa Jeshi la Magereza na Vyuo vya
Mafunzo. Nina imani kuwa
mchanganyiko wa masomo ya Uongozi na Utawala Bora, Usimamizi wa Fedha,
Sheria, Ugavi, Haki za Binadamu, Ustawi wa Jamii na Afya umewajengea
msingi bora katika kusimamia shughuli za kila siku za uendeshaji wa
Jeshi la Magereza na Vyuo vya Mafunzo.
Wito wangu kwenu wahitimu ni kuwataka muende saa katika vituo vyenu kuyatekeleza mambo yote muhimu mliyojifunza hapa Chuoni.
Katika
kuzingatia Haki za Binadamu duniani, vyombo vya Dola kama vile Magereza
vinaangaliwa sana ili kuona ni kwa kiasi gani nchi husika inakiuka au
inazingatia na kutekeleza Misingi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Nimefurahi kusikia nanyi kwenye mafunzo yenu mmejifunza kwa kina mambo hayo. Hivyo,
nawataka Maafisa mnaohitimu leo na wale walioko kazini wakati wa
kutekeleza majukumu yenu mzingatie Sheria, Kanuni , Haki za Binadamu na
Utawala Bora.
Nidhamu katika kazi ndiyo msingi wa maendeleo ya mfanyakazi na Taasisi anayoifanyia kazi. Katika Uaskari kiwango cha Nidhamu kinachotakiwa ni cha hali ya juu. Hivyo, ninawaasa wahitimu wakazingatie Nidhamu katika utendaji kazi wao wa kila siku. Kwani
kufanya hivyo kutawafanya kuwa Maofisa bora na hata waliochini yenu
mtawasimamia vizuri na hatimaye kulipa sifa Jeshi la Magereza na Taifa
kwa ujumla.
Suala lingine ambalo ninapenda kuwaasa wahitimu ni juu ya mapambano dhidi ya UKIMWI. Ieleweke wazi kwamba sera ya Taifa hivi sasa ni kuwataka wananchi wapime kwa hiari kujua afya zao. Hivyo
nami natoa wito kwenu wahitimu mjenge tabia ya kupima afya zenu kwa
hiari siyo unangoja hadi ugonjwa umekuzidi ndiyo unaenda kupimwa, na pia
mkawahimize waliochini yenu kupima afya zao.
Napenda
pia kumpongeza Mkuu wa Chuo na uongozi wote wa Chuo hiki kuweza
kufanikisha majukumu yake katika mazingira magumu yaliyopo. Risala yako
na ile ya wahitimu zimetaja changamoto mbalimbali zinazozorotesha
utendaji kwa kazi. Lakini
nimefurahishwa kusikia kwamba pamoja na changamoto hizo, mafunzo
yameweza kufanyika kwa kiwango kinachotakiwa. Juhudi zenu zinastahili
sifa na ninawaomba mziendeleze wakati hatua za kuboresha hali iliyopo
zinaendelea kuchukuliwa. Serikali kwa upande wake itaendelea kutatua changamoto hizo kadiri fursa itakapokuwa inapatikana.
Nawapongeza wahitimu kwa kuweza kumaliza mafunzo yenu kwa mafanikio licha ya mapungufu mliyokutana nayo. Kwa kulitambua hilo, nawapongeza zaidi kwa moyo wenu wa kujitolea kwa kuonesha njia ya kuchangia shilingi milioni moja, laki mbili na ishirini elfu (1,220,000/=) kwa ajili ya ukarabati wa mfumo wa kuingiza maji safi kwenye mabweni matatu.
Mwisho,
nawashukuru wote waliofanikisha shughuli hii, bila ya kuvisahau vikundi
vya Sanaa na Utamaduni kwa burudani nzuri na yenye maudhui.
Baada ya kusema hayo,
NATAMKA
KWAMBA WAHITIMU WOTE 244 WA KOZI YA UONGOZI WA NGAZI YA JUU WAMEFAULU
NA KUSTAHIKI KUTUNUKIWA CHEO CHA MRAKIBU MSAIDIZI WA MAGEREZA NA
KUFUNGWA RASMI.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment