Mh. Vincent Josephat Nyerere (MB) Waziri Kivuli Mambo ya Ndani CHADEMA |
Ndugu
wanahabari, kwanza kabisa napenda kuwashukuru kwa kuitikia wito wangu,
ili niweze kuzungumza na watanzania kupitia kwenu kuhusu hatari kubwa
inayolikumba taifa ya madawa ya kulevya.
Biashara
haramu ya dawa za kulevya imekua kwa kasi sana hapa nchini miaka ya
hivi karibuni licha ya kuwa na vyombo lukuki vya ulinzi na usalama na
licha ya kuwa na Tume maalumu ya kudhibiti madawa ya kulevya chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa
mujibu wa Taarifa ya Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda, iliyosomwa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera Uratibu na Bunge Mhe. Wiliam
Lukuvi tarehe 26 Juni, 2013 siku ya maadhimisho ya kitaifa ya kupiga
vita dawa za kulevya huko Dodoma ni kwamba katika kipindi cha mwaka 2008
hadi 2012 watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na biashara
haramu ya dawa za kulevya hapa nchini. Aidha, watanzania wapatao 240
walikamatwa na madawa ya kulevya katika nchi za Brazil, Pakistan na
Afrika ya kusini na hivyo kutia doa taswira ya Tanzania katika jumuiya
ya kimataifa. Kutokana na kukithiri kwa biashara hii haramu, Serikali
kupitia maadhimisho hayo ya siku ya kupiga vita madawa ya kulevya
duniani ilitangaza kuwa biashara ya dawa za kulevya kuwa ni janga la
taifa.
Mtakumbuka
pia kwamba hivi majuzi, muda mfupi baada ya Serikali kutangaza kuwa
biashara ya dawa za kulevya ni janga la taifa , walikamatwa wasichana
wawili ambao ni watanzania huko Afrika ya kusini wakiwa na kilo 150 za
madawa ya kulevya yenye thamani ya zaidi ya randi milioni 42.6 sawa na
zaidi ya shilingi bilioni 6 za kitanzania.
Ndugu
wanahabari, matukio yote haya yametokea ndani ya kipindi cha miaka sita
tu ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne ambapo kuna viongozi wa juu
Serikalini ambao waliwahi kusema kuwa wanawajua watu wanaojishughulisha
na biashara haramu ya dawa za kulevya lakini mpaka sasa hawajawataja
wahusika na wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahusika.
Ndugu
wana habari, miongoni mwa viongozi wa serikali na taasisi nyingine
waliosema kuwa wanawafahamu wafanya biashara ya madawa ya kulevya ni:-
Rais
Jakaya Kikwete, ambaye alipiga hatua kubwa zaidi na kusema anawajua
hata viongozi wa dini wanaofanya biashara hiyo. Licha ya maaskofu na
viongozi wengine wa dini kumtaka Rais awataje wahusika hao wa madawa ya
kulevya ili kuuweka ukweli wazi, Rais hajafanya hivyo mpaka sasa.
Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya:
huyu alisema anayo majina ya vigogo (kwa maana ya viongozi)
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini hajaweka majina
hayo hadharani na wala haijulikani kama wahusika hao wamechukuliwa hatua
yoyote hadi sasa.
Mbunge wa Mwibara
– Kange Lugola alisema katika bunge la bajeti 2013/2014 kuwa kama Rais
na Kamishna wa tume ya kudhibiti dawa za kulevya wanawajua “kwa majina”
watu wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya na hawataki kuwataja
watu hao wala kuwachulia hatu yamkini watu hao ni miongoni mwa mawaziri
ndio maana kuna kigugumizi cha kuwataja na kuwachukulia hatua. Tangu
Mhe. Kange Lugola alihusishe baraza la Mawaziri na kashfa hiyo ya
kuhusika na biashara ya dawa za kulevya hakuna hatua yoyote
ilivyochuliwa na Serikali kuthibitisha au kubatilisha kauli hiyo.
Mwenyekiti
wa Makampuni ya IPP Bw. Reginald Mengi aliwahi kutoa taarifa ya wazi
kuwa kuna kundi la matajiri wanaoshirikiana na viongozi wa Jeshi la
Polisi waliokuwa wanapanga njama za kumwekea mtoto wake dawa za kulevya
ili wambambikizie kesi ya dawa za kulevya na hivyo kuchafua heshima ya
Bw. Mengi na familia yake. Ndugu mengi alisisitiza katika taarifa yake
kwamba yuko tayari kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na mamlaka
nyingine zinazohusika ili kubaini njama hizo na kuchukua hatua stahiki
kwa wahusika lakini mpaka leo Ndugu Mengi hakuhojiwa ili kuthibitisha
kauli yake jambo linaloashiria kwamba kuna ukweli katika kauli yake.
Baada
ya matukio yote haya na baada ya Serikali kukaa kimya kuhusu matukio
hayo, mimi kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kwa niaba ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ninatoa tamko kama ifuatavyo:
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete awataje na kuwachukulia hatua watu aliosema
anawafahamu wanaojishughulisha na biashara ya dawa za kulevya la sivyo
akubali kubeba shutuma kwamba Serikali yake ndio Mratibu Mkuu wa
biashara ya dawa za kulevya ndio maana anashindwa kuchukua hatua.
Kamishana
wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya awajibike kwa kutoa maelezo kwa
umma juu ya hatua alizochukua dhidi ya wahusika wa biashara ya dawa za
kulevya aloiosema anawafahamu la sivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
italazimika kuwashawishi wananchi kuamini kwamba yamkini na yeye yumo
katika mtandao wa wafanya biashara haramu ya dawa za kulevya ndio maana
anasita kuwachukulia hatua wahusika hao ambao alishakiri kuwa
anawafahamu.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege awajibike kwa kutoa maelezo kwa
umma kuwa ni tatizo gani linaloikabili mamlaka yake hadi kufanya viwanja
vya ndege vya Tanzania kuwa ndio njia rahisi ya kuingiza na
kusafirishia madawa ya kulevya katika ukanda wa Afrika Mashariki?
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi
wawajibike kwa kutoa maelezo kwa umma kuwa ni kazi ipi wanayofanya
ikiwa madawa ya kulevya yanaingizwa nchini na kusafirishwa nje ya nchi
kwa kasi kubwa zaidi?
HITIMISHO: Ni
vema kama taifa tukatambua madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana wetu
ambao ndio nguvu kazi ya taifa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa
wahusika wa dawa za kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu
kazi ya taifa ikishaharibiwa na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo
Serikali ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia macho jambo hili kwa
manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu taifa na huo ni usaliti dhidi
ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na kusimamia usitawi wa
wananchi wa Tanzania. Aidha, Serikali itambue pia kwamba kuendelea kukaa
kimya bila kuchukua hatua yoyote juu ya jambo hili kunatoa dalili
kwamba yamkini ya yenyewe inahusika na biashara hiyo.
MUHIMU:
IKIWA SERIKALI ITAENDELEA KUPUUZIA JAMBO HILI AMBALO LINALIANGAMIZA
TAIFA, BASI KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI ITAENDESHA OPERESHENI NCHI
NZIMA ILI WANANCHI WAPIGE KURA KWA WAHUSIKA WAKUU WA BIASHARA YA DAWA
ZA KULEVYA, NA BAADA YA ZOEZI HILO, TUTAANIKA HADHARANI (KWA KUWATAJA
MAJINA) WAHUSIKA WA BIASHARA HARAMU YA DAWA ZA KULEVYA.
No comments:
Post a Comment