Wafanyabiashara changamkia
ujio wa Obama
Rais Barack Obama anawasili nchini kesho kwa ziara ya siku mbili. Pamoja na kufuatana na familia yake, Rais huyo pia ataongoza ujumbe wa watu zaidi ya 700 wengi wao wakiwa wafanyabiashara wakubwa wanaotafuta fursa za uwekezaji hapa nchini.
Hivyo, asijidanganye mtu kwamba Rais Obama na
ujumbe wake wa wafanyabiashara wanakuja nchini kupiga siasa au kuimbiwa
ngonjera na taarabu. Wala asijidanganye mtu kwamba Marekani imefanya
madhumuni ya ziara hiyo kama siri kubwa ili nchi hiyo iweze kuwazuga na
kuwahadaa viongozi wetu kwa lengo la kuchukua rasilimali zetu kirahisi.
Marekani tayari imeitangazia dunia na wananchi wa
Marekani waliokuwa wakiikosoa ziara hiyo wakidai ingekuwa mzigo kwa
walipa kodi wa nchi hiyo, kwamba ziara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa
Marekani na kwamba nchi hiyo ilifanya makosa makubwa kuiachia China
kujitanua na kujiimarisha barani Afrika kwa kuingia mikataba ya kiuchumi
na nchi mbalimbali. Ziara ya Rais Xi Jinping wa China nchini Tanzania
hivi karibuni pia imeizindua Marekani kutoka usingizini, hivyo kaulimbiu
ya Marekani hivi sasa ni ‘kutangulia sio kufika’.
Watanzania tunapaswa kuuona ujio wa Rais Obama na
ujumbe wake katika muktadha huo. Ni ujio wa kibiashara na kiuchumi ambao
Serikali na wafanyabiashara wetu wakijipanga vizuri na kutanguliza
weledi na uzalendo nchi yetu nayo itafaidika na ziara hiyo. Katika
mazungumzo na mapatano na ujumbe huo kabla ya kusaini mikataba, mkakati
wetu kitaifa uwe ‘nipe nikupe’ na tusikubali hata kidogo kuingia tena
mikataba ya ghiliba na ya ujanjaujanja.
Jambo muhimu hivi sasa ni kuwauliza
wafanyabiashara na viongozi wa Serikali jinsi walivyojipanga kuingia
katika mazungumzo na ujumbe huo. Tusijidanganye. Ujumbe wa Rais Obama
utakuwa na wataalamu wa hali ya juu wa mapatano ya kibiashara za
kimataifa (international trade negotiators).
Kwa kawaida, wengi wao huwa ni maprofesa
waliobobea wa vyuo vikuu ambao wana nadharia na ujuzi mkubwa katika kile
kinachoitwa mchezo wa mapatano (negotiation game). Hivyo, Wamarekani
wataingia kwenye mapatano wakiwa tayari wanajua watoe nini na wachukue
nini, kwa maana ya kutawala mchakato mzima na kujua ni wakati gani
wasonge mbele au warudi nyuma.
Ni wazi kwamba itakuwa balaa kubwa kwa nchi yetu
iwapo wawakilishi wetu wataingia katika mazungumzo hayo kichwakichwa.
Tatizo tunaloliona hapa ni kwamba mazungumzo hayo yatahusu pia masuala
yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu, yakiwamo uchimbaji wa gesi,
mafuta, urani na madini. Sisi hatuna wataalamu wazalendo waliobobea
katika nyanja hizo, hivyo tunaishauri Serikali isione haya kutafuta
washauri mabingwa waelekezi ambao ni waaminifu na waadilifu ili
washiriki katika mazungumzo hayo.
Huu sasa ni wakati mwafaka kwa nchi yetu kutumia
ushindani wa kibiashara kati ya Marekani na China ili tunufaike.
Serikali ijipange vizuri kuweka wazi sera za nchi kuhusu biashara ya nje
na matumizi ya rasilimali zetu na itayarishe maeneo ambayo tayari
imetenga kwa wawekezaji.
Ni matarajio yetu kwamba wafanyabiashara wetu
katika sekta binafsi katika nyanja za utalii, biashara na viwanda nao
watajipanga vyema kukutana na wenzao kutoka Marekani. Jambo wanalopaswa
kuzingatia ni kwamba ujumbe wa Rais Obama unakuja nchini kutafuta fursa
za kibiashara na kiuchumi na siyo vinginevyo.
No comments:
Post a Comment