Sunday, 30 June 2013

Ulinzi Mkali wa Ujio wa Obama:

Watanzania Wasikwazike 

au Kufedheheka na 

Ulinzi Mkali wa Ujio wa Obama: Ni kawaida...


Afisa wa Kitengo Maalum cha Ulinzi wa Rais akisimama helikopta ya Rais ikiondoka

Ulinzi mkali ambao tayari upo na utazidi kuonekana wakati wa Ujio wa Rais wa Marekani umewafanya baadhi ya Watanzania kujihisi wanadunishwa au kuabishwa. Wapo wengine ambao wanaona kuwa hatua mbalimbali za kiusalama zinazochukuliwa kumlinda Obama, Familia yake na ujumbe wake zinaonesha dharau na kutoaminiwa kwa vyombo vyetu vya ulinzi. Wengine wanafika mahali pa kuhisi kuwa Wamarekani wanatudharau sana kiasi kwamba wanatuchagulia nani aonene na Obama (rejea taarifa kwenye gazeti la Mwananchi la leo). Watanzania hawapaswi kujisikia hivyo hata kidogo.

Ulinzi wa Obama ni Mkali iwe ndani ya Marekani au Nje

Wakati wowote Rais wa Marekani anaposafiri iwe ndani ya Marekani au nje ya Marekani ulinzi wake ni mkali na karibu kamili (almost absolute). Kuanzia angalia ambalo anakuwepo (linakuwa no fly zone) na kuwa anaenda na kila kitu kinachoweza kutumika wakati wowote wa dharura yoyote inayoweza kufikirika kutokea. Kuanzia majanga ya moto, maji, maandamano ya kisiasa au hata mapinduzi ya kijeshi ulinzi wa Rais wa Marekani umejiandaa.

Mfano mzuri ni kuwa ikulu ya Rais pale DC – Jumba Jeupe – juu kabisa kuna mzinga wa kutungua ndege – surface to air battery. Lakini kubwa zaidi ni kuwa anga lote linalozunguka Ikulu hiyo ni eneo ambalo ndege haziruhusiwi kuruka (prohibited airspace). Na wakati wowote Rais anaposafiri mahali popote ndege haziruhusiwi kuruka juu yake. Anapotua kwenye uwanja kwa mfano hapa Detroit, hakuna ndege nyingine itakuwa inatua wakati huo huo! Sasa kama hili linatokea Marekani kwa kiasi gani linaweza kutokea Tanzania?

Ripoti hii maalum basi ina lengo la kuwasaidia Watanzania kutokwazika na kiasi cha ulinzi ambao Obama anakuja nao pamoja na usumbufu unaotokana na hilo. Kama msafara wa Rais Kikwete huwa unazusha usumbufu kwa watu basi wa Obama utasababisha kadhia – chukua msafara wa Kikwete zidisha mara 1000!

Mambo ya Kawaida ya Ulinzi wa Rais

Kwa yeye kuwa Rais wa Marekani Obama anapatiwa ulinzi wa hali ya juu kabisa labda wa kiongozi mwingine yeyote duniani. Anapokuwa ndani ya Marekani anapata bado ulinzi wa hali ya juu lakini pia ni kama mara ishirini hivi chini ya ulinzi anaopata akiwa nje ya Marekani. Hii ni kwa sababu moja kubwa anapokuwa Marekani anakuwa katika ulinzi wa vyombo vingi sana vya nyumbani na mahali popote anapokwenda. Hivyo, vitu kama magari watu, n.k vingi vinakuwa ‘mobilized’ kutoka ndani.


Ulinzi huu wa kawaida ni ule ambao mara nyingi watu wanaona (maafisa wa Usalama wanaoambatana na Obama popote anapokwenda) na ule ambao uko kwenye kivuli (usionekana) ambao unahusisha wataalamu wa mambo ya mawasiliano, wapelelezi, majasusi n.k

Rais wa Marekani anapotoka nje ya nchi anaenda pamoja na kikosi cha maaskari wasiopungua 500 hivi! Ulinzi wa Rais wetu huwa ni kama watu 40 hivi maafisa wa usalama na anapoenda nje namba hiyo inapungua kidogo. Tunaposema anakuja na watu 500 hivi kwa ajili ya ulinzi hawa ni nje ya wale wanaotangulia na wale ambao taifa husika linatoa. Kati ya hao walinzi kama 200 hivi ni makomandoo watupu wa jeshi la Marekani na Taasisi za kijasusi.
Rais Obama anaposafiri anasafiri na madaktari bingwa wasiopungua sita hivi pamoja na wapishi wake pamoja na choo chake! Pamoja na hao anaambatana na manesi na wataalamu mbalimbali wa afya ambao wanaweza kuingia kazini wakati wowote. Anapokuwa Washington DC hospitali moja iko maalum kwa ajili ya dharura ya Rais tu na ina mlango wake ambapo likitokea jambo basi Rais hatopata shida ya kuzungushwa! Pamoja na hivyo kuna kiasi cha lita za damu aina AB (damu ya Obama) ambayo pia inasafiri naye mahali popote kwa ajili ya dharura yoyote itakayohitaji kuwekewa damu. Hii ni ndani au nje ya Marekani.
Ndege ya Obama ni chombo cha ulinzi wake pia
Ndege ya Rais wa Marekani maarufu kama Air Force One siyo ndege kama ndege nyingine. Ni ndege ambayo imetengenezwa kuhakikisha kuwa Rais anapokuwa angani anakuwa salama kabisa. Imeundwa kuweza kuhimili vishindo vya mlipuko wa Nyuklia katika umbali ambao inakuwa inaruka na mabawa yake hayapigiki risasi (armor plated). Ndege hiyo pia ina uwezo wa kuingilia mawasiliano ya rada ya nchi yeyote inaporuka (radar jamming) na pia inasafiri ikiwa na makanyaboya ya mizingi ya ardhini (earth to air missiles). Ndege hiyo ina namba za simu zisizopungua 85 ambazo zinatumika wakati wote kuhakikisha kuwa Rais anaweza kuwasiliana na mtu yeyote hata anapokuwa angani.
 Obama katika ofisi yake angani
Anapokuwa ardhini helikopta za jeshi la Majini ambazo zinafuatana na rais nazo zinakuwa tayari kwa dharura yoyote. Rais wa Marekani ana helikopta 19 hivi ambazo zinaweza kutumiwa mahali popote. Hivyo, kwa mfano magari na helikopta zilizotumika Senegal si lazima zije Tanzania zinaweza kurudishwa Marekani wakati nyingine zikija Tanzania. Hili ni kweli pia kwa magari. KUtokana na ukaribu wa Afrika ya kusini na Tanzania bila ya shaka baadhi ya raslimali za ulinzi zilizotumika Afrika ya Kusini zitaletwa Tanzania vile vile.
Marine One – chopa ya Rais
Anasindikizwa na Meli za Kivita
Anapokuwa nje ya Marekani Rais wa Marekani anasindikizwa na meli za kivita zinazopokezana majukumu kwa kadiri anavyozunguka dunia na zinakuwa tayari wakati wote kuingilia kati ikibidi. Meli hizi zimejaa wanamaji na wapiganaji wa jeshi la majini (Marines). Wapiganaji wa meli hizi wako tayari wakati wowote kuingia kwenye nchi yoyote kumuokoa Rais wao endapo kuna tishio la maisha yake.
Gari lake nalo ni chombo cha ulinzi
Bila ya shaka katika ya vyombo vya ulinzi wa karibu kabisa kwa Rais ni gari lake analotumia ambalo limetengenezwa maalum kwa ajili ya kumpatia ulinzi wa hali ya juu. Hii ni pamoja na kuzuia risasi na milipuko ya mabomu ya mkono au rocket launcher! Na huwa hali moja bali kadhaa ili kuhakikisha watu hawajui Rais anakuwa katika gari gani hasa.


Limo – full armored

Rais anapokuwa ndani ya nchi nyingine
Rais wa Marekani anapokuwa ndani ya nchi nyingine suala la usalama linakuwa kwa kiasi kikubwa mikononi mwa nchi husika – kiufundi tu. Kimsingi hata hivyo ulinzi wake unahakikishiwa na Marekani na vyombo vyake vya ulinzi. Nchi husika na vyombo vyake vya ulinzi vinakuwa na mawasiliano ya mipango na hawa Wamarekani. Kutegemeana na nchi nan chi baadhi ya nchi zinaruhusiwa kwa kiasi kikubwa na nchi nyingine zinaona ni bora kuwaachia Wamarekani waendeshe ulinzi wenyewe – ili kukwepa lawama. Hivyo, Obama akienda Israeli kwa mfano walinzi wa Kiisraeli wanapewa nafasi kubwa kuliko kwa mfano akienda Afghanistan!



Lakini popote anapokwenda nchi husika inakuwa nyuma ya Wamarekani katika masuala ya ulinzi. Hili ni muhimu kulizingatia hasa kwa wale ambao wanaweza kudhani kuwa kwa kusisitiza kuwa Wamarekani wasimamie ulinzi wa Obama akiwa Tanzania basi Wamarekani wametudharau. Hili si kweli. Wamarekani wanatoa ulinzi huu wakishirikiana na watu wetu lakini kutokana na uzito wa ujumbe wenyewe na hasa hali ya usalama katika eneo letu (ikumbukwe tayari kulishatokea milipuko dhidi ya Wamarekani na wapo wenye kuvionea huruma vikundi vya kighaidi) ni wazi kuwa Wamarekani watakuwa na sharti la kusimamia ulinzi wote wao wenyewe na hilo sisi wengine tushukuru tu na labda kujifunza.



Japo wengi watauona ule ulinzi ulioko kwenye msafara ambao kwa kweli ni kidogo tu – ulinzi wenyewe ni ule ambao uko nje ya msafara; watakuwa kwenye mapaa, kwenye mahoteli, kwenye barabara na wengine watakuwa katikati ya watu wamechanganyika. Fikiria kwa mfano alipoenda India kiasi cha ulinzi kilikuwa karibu maafisa 10,000 wakitengeneza kama ngazi tano za ulinzi – na ninaamini hili litatokea Tanzania pia. Kulikuwa na watu karibu 1000 kwenye ziara ya India ambao walikuwa wanamlinda Obama ambao ni Wamarekani watupu!

Baadhi ya maafisa wanaomlinda Obama wanavaa miwani zenye camera ambazo zinarekodi na kurusha moja kwa moja sura na watu mbalimbali anaokutana nao au wanaojitokeza kumpokea. Yote ni katika kuhakikisha usalama

Kwenye njia zote ambao Obama na mke wake watakuwepo kutakuwepo na walenga shabaha (snipers) na majasusi wakitoa ulinzi. Kama Obama atalala Ikulu basi kutakuwa na maofisa wa Kimarekani wasiopungua 2000 hivi kuongeza ulinzi wa Ikulu yetu na kufanya Ikulu hiyo kuwa jengo salama zaidi duniani kwa usiku huo! Hili litakuwa pia kweli kama atalala kwenye mojawapo ya mahoteli yetu makubwa Jijini Dar. Kwenye nchi nyingine ambazo Rais hawezi kulala kwenye nchi husika basi meli ya kijeshi ya Kimarekani iliyoko karibu inageuzwa kuwa hoteli na wakati mwingine atalala angani wakati anarejea kwao!

Njia zote zina mbadala wake

Njia zote ambazo Obama atapitia tayari zitakuwa na mbadala waka (alternative routes) kiasi kwamba jambo moja likitokea kwenye njia moja tayari wanajua ni njia gani nyingine wachukue. Ni kwa sababu hiyo labda watu wa Dar-es-Salaam wameshauriwa kuangalia kama wanasababu ya kwenda mjini. Usumbufu wa aina hiyo hautatokea Dar tu na watu wakakwazika hata anapokuwa hapa usumbufu huo wengine tunaupata.


Mara mbili nimewahi kujikuta katikati ya mahali ambapo Rais anasafiri au kuja. Mara ya kwanza ilikuwa mara baada ya tukio la Septamba 11 wiki chache baadaye Rais Bush alikuja Detroit na alikuwa na mkutano hoteli moja iliyokuwa upande wa pili wa hoteli ambayo nilikuwa nafanyia kazi. Wakati huo nikifanya kazi kwenye mambo ya corporate reservations. Wiki kadhaa nyuma maajenti wa SS walikuja na kubook sakafu nzima ambayo haturukuhusiwa kumweka mtu yeyote!

Mara ya pili mwaka jana wakati wa kampeni katika misafara yangu nikajikuta nabadilishiwa njia mahali ambapo palikuwa pamejaa mapolisi na barabara imefungwa – kisa Obama alikuwa na chakula cha jioni nyumbani kwa mtu mmoja wa wafadhili wake!

Hivyo, Watanzania wanapopata ugeni huu wasikwazike sana kama mawasiliano yao yataingiliwa – hasa wanaoishi Dar kwa sababu ya kuhakikisha kuwa hakuna bomu linaloweza kulipuliwa kwa simu – na hata kupata usumbufu mkubwa. Obama anakuja akiwakilisha taifa lenye nguvu kubwa zaidi duniani; nguvu hii kwa kiasi tu Watanzania wataiona na itawasumbua. Kwa wale wanaofikiria labda Obama ni kama Rais wa China wafikirie tena; ulinzi wa Obama ni mara nyingi zaidi ya ulinzi wa Xi Jinping.

Kwa hiyo kama ulishaanza kukwazika na kuona umedharauliwa hauna sababu tena; shangaa, furahia, jifunze na ombea aje na kuondoka salama yeye na msafara wake wote. Wakishaondoka, pumua kwa furaha.

Waandishi wa Tanzania na Watanzania wasiogope kuwapiga picha aafisa wa usalama wakiwa kazini. Hakikisha tu kwamba ukifanya hivyo huwawekei kizuizi wakiwa kazini.

No comments:

Post a Comment