Saturday, 8 June 2013

Uchimbaji wa urani


 
Uchimbaji wa urani kuanza karibuni

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesisitiza kuwa mpango wa kuchimba madini ya urani bado uko palepale na kwamba hiyo inatokana na Serikali kujiridhisha na hatua zote.
Profesa Muhongo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na watalaamu kutoka Umoja wa Ulaya (EU), kuhusu namna ya kutekeleza uchimbaji huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Alisema mpango huo utatekelezwa baada ya kukamilika kwa taratibu zote muhimu.
Waziri huyo alisema Serikali imejiridhisha kwamba madini hayo hayatakuwa na madhara na kwamba tahadhari zote muhimu zimeshachukuliwa.
URANI
Alisema hatua hizo zimefanywa huku kukiwa na upotoshaji unaoenezwa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya nchi.
“Madini hayo yatachimbwa kama tulivyopanga na hatua zote stahiki zimeshachukuliwa kuhusu jambo hilo. Nawaomba wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya mpango huu,”
alisema Profesa Muhongo.
Aliwataka wananchi wapuuzie upotoshaji unaoenezwa dhidi ya mpango wa kuchimba madini hayo utakaofanywa na Kampuni ya Mantara, kuwa utakuwa na madhara kwa binadamu.
Kwa upande wake, Balozi wa EU nchini, Fillberto Sebregond
alisema wamejipanga ipasavyo kuhakikisha kuwa uchimbaji huo unakwenda vizuri na bila madhara kwa binadamu.
Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inapata mapato yatakayotokana na uuzaji wa madini hayo.
“Tuna ushirikiano mzuri na nchi hii na tutasaidia maeneo yote yatakayochimbwa madini hayo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi katika hali ya usalama na bila madhara yoyote,” alisema Balozi Sebregond .
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mantara, Asa Mwaipopo alisema kazi ya kuchimba madini hayo katika eneo la Mkuyu wilayani Namtumbo, inatarajia kuanza hivi karibuni. Alisema kazi hiyo imepangwa kuanza katika kipindi hiki cha kiangazi kwa sababu wakati wa masika maeneo hayo yanakuwa na matatizo.

No comments:

Post a Comment