Monday, 3 June 2013

UBORESHAJI WA ELIMU TANZANIA

“Serikali itaimarisha ukuzaji, uboreshaji na utekelezaji wa mitalaa kwa kuzingatia mahitaji ya taifa na ya walengwa katika ngazi zote za elimu na mafunzo”.
Inasema pia kuwa, Serikali itaimarisha usimamiaji na upimaji wa utekelezaji wa mitalaa  katika taasisi za elimu na mafunzo katika ngazi zote ili kuleta ufanisi wa elimu na mafunzo yatolewayo.
Miundo na taratibu za elimu na mafunzo
Bora elimu bora nasi bora elimu
Rasimu hiyo inasema kuwa, pamoja na kwamba taifa limeendelea kutekeleza muundo wa kitaaluma wa 2-7-4-2-3+, na muundo wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi wa 2-7-4-1+, haiingiliani kwa urahisi.
“Wapo wahitimu wa darasa la saba wanaojiunga na mafunzo ya ufundi stadi lakini mwendelezo wao haupo kwenye miundo iliyopo,” inasema.
“Hali hii imesababisha kutokuwa na muunganiko, ulinganifu na mtiririko mzuri katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo na hivyo kusababisha wahitimu kukosa mwendelezo katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo na wengine kutokuwa na mwelekeo.”
Rasimu hiyo inasema kuwa, lengo ni kuwa na mfumo, miundo na taratibu nyumbufu za elimu na mafunzo na kuleta tija na ufanisi.
“Serikali itaweka mfumo, miundo na taratibu nyumbufu katika elimu na mafunzo ili kuleta ulinganifu, muunganiko na ufanisi wa ngazi na fani mbalimbali za kitaaluma na kitaalamu kumwezesha mwanafunzi kutoka mkondo mmoja kwenda mwingine, inasema.
Umri wa kuanza shule
Katika suala la umri wa kuanza shule, rasimu hiyo inasema kuwa muundo wa elimu na mafunzo uliopo unatoa fursa ya mtoto mwenye umri wa miaka mitano kujiunga na elimu ya awali kwa miaka miwili.
“Mtalaa wa elimu ya awali umetengenezwa kwa namna ambayo unatakiwa ufundishwe kwa miaka miwili, utafiti unaonyesha mtalaa huo unaweza kufundishwa kwa mwaka mmoja.”
Inasema elimu ya awali haizingatii mahitaji maalumu ya baadhi ya watoto.
Itifaki ya Dakar ya mwaka 1999 ambayo Tanzania imeridhia, elimu ya awali inatakiwa kuwa kati ya umri wa miaka mitatu hadi sita.
Inasema kuwa, elimu ya lazima kwa sasa ni darasa la saba na wahitimu wake katika mfumo wa sasa wanakuwa na umri wa miaka 13.
“Wahitimu hawa wanakuwa na umri mdogo na hawana maarifa na ujuzi unaotosheleza kujiunga na ulimwengu wa kazi au kukabiliana na changamoto za maendeleo iwapo watakosa fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari ngazi ya kawaida,”:
“Pia muda wa kusoma katika ngazi nyingine umeendelea kutokuwa na falsafa ya kuongoza suala hili na hivyo kutokuwa na ulinganifu na mwingiliano fanisi.”
Kutokana na mambo hayo, rasimu hiyo inasema lengo la serikali ni kurekebisha muda wa elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali.
“Serikali itaweka utaratibu wa elimu ya awali kuwa ya lazima na kutolewa kwa watoto wenye umri kati ya miaka mitatu hadi mitano kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja,”
“ Elimu ya msingi kuwa ya lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne; na kutolewa kwa miaka kumi na umri wa kuanza darasa la kwanza kuwa kati ya miaka minne hadi sita kulingana na maendeleo na uwezo wa mtoto kumudu masomo katika ngazi husika.”
Inasema kuwa, Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha muda wa kukamilisha elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali za elimu baada ya Elimu  ya Msingi unakuwa na tija na ufanisi.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, malengo mahsusi ya Sera ni hiyo ni kuwa na mfumo, miundo na taratibu nyumbufu kumwezesha Mtanzania kujiendeleza kwa njia mbalimbali katika mikondo ya kitaaluma na kitaalamu.
Pia kumpa elimu na mafunzo yenye viwango vya ubora unaotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa



No comments:

Post a Comment