Friday, 16 August 2013

Vurugu Bagamoyo




Vurugu Bagamoyo zajeruhi,

 nyumba zachomwa moto



. Madereva wa malori (fuso) na wananchi wamezusha vurugu kubwa Kitongoji cha Kweishala (Mnara wa Voda), Kata ya Mbwewe Wilaya ya Bagamoyo na kusababisha watu kujeruhiwa huku nyumba zaidi ya sita, hoteli ndogo na pikipiki moja kuteketezwa  kwa moto, na baadhi ya wanakijiji wakidaiwa kukimbia makazi yao wakihofia kuuawa.
Vurugu hizo zilianza alfajiri Agosti 15 baada ya gari aina ya Fuso liliokuwa limebeba shehena ya marobota 189 ya nguo za mitumba na 68 ya viatu kuacha njia na kupinduka  eneo la kijiji hicho, ambapo baadhi ya wakazi wa eneo hilo walivamia gari hilo na kudaiwa kupora mizigo na kuihifadhi katika nyumba zao.
Baada ya tiko hilo, Polisi wa Kituo cha Chalinze walilazimika kwenda kuongeza nguvu kutuliza ghasia hizo kutokana na wenzao wa Kituo cha Mbwewe kuzidiwa.
Katika vurugu hizo kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 15 alijeruhiwa na polisi walifanikiwa kukamata watu watatu waliohusika na tukio hilo.
Diwani wa  Kata ya Mbwewe, Omar Mhando na Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Mashaka Kigoko walisema baada ya Fuso hilo kuanguka, lililala katikati ya barabara na kusababisha magari mengine yaliyokuwa yakisafiri katika barabara kuu ya Chalinze-Segera kushindwa kuendelea na safari kwa zaidi ya saa nne, hali ambayo iliwalazimu madereva kujikusanya pamoja ili kuwapa msaada wenzao.
“Chanzo cha huu mkasa ni hilo Fuso lililoanguka na shehena ya mitumba na viatu, ilikatisha barabara na kuziba njia hivyo magari mengine yalipofika hapo yalikwama, na muda ulivyozidi waliamua kushuka na kufuatilia kulikoni na kukuta wenzao wamepata ajali,lakini badala ya kusaidiwa kutoka garini watu walivamia na kupora mali,” alisema Mhando.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi amethibitisha tukio hilo na  kuwa hadi saa tisa alasiri jana wanakijiji sita ndiyo walioripotiwa kujeruhiwa.

No comments:

Post a Comment