Friday, 14 June 2013

Mzanzibari mpinga utumwa




 Springfield Mzanzibari mpinga utumwa

 
ZANZIBAR



 


Leo tunamzungumzia Mzanzibari na Mwafrika wa kwanza, John Springfield ambaye aliishi Guilford, Uingereza baada ya kufanyakazi melini, kuendesha kampeni ya kuzuia utumwa, na hatimaye kuwa mwalimu wa kushona viatu katika Shule ya Robert Macdonald’s Guildford Mission Industrial School, nchini Uingereza.
Alizaliwa 1 Julai 1847, mtoto wa Chifu Jumbalowagee kule Zanzibar. Akiwa msituni akichuma matunda katika umri wa miaka tisa, alitekwa nyara na Wareno ambao baadaye waligundua kuwa alikuwa bado mdogo kwa umri kuingizwa utumwani.
Taarifa zinabainisha kwamba aliokolewa na mwanamke ingawa nyingine zinasema Dk Livingstone ndiye aliyemwokoa na kumtia kwenye ajira ya meli yake HMS Victoria. Ila asingeweza tena kurudi kwao kwa vile aliingizwa kwenye shughuli za utumwa na kula mkate (chakula cha Wazungu) na kusahau utamaduni wake.
Jina lake la asili halijulikani, lakini alipewa jina la John Springfield. Baada ya hapo akawa anafanyakazi kwenye meli hiyo ya HMS Victoria. Aliacha kazi na kwenda Amerika kuhubiri mapambano ya kuzuia biashara ya utumwa.
Kampeni yake dhidi ya utumwa kule Amerika haikupokelewa vizuri na akaamua kurudi tena Uingereza ambako mwaka 1870 alimuoa mama wa kizungu aliyeitwa Eliza Andrews ambaye alikuwa mtoto wa Williama Adrews aliyekuwa mtunza bustani.
John na Eliza walimzaa mtoto mmoja wa kike waliyemwita Miriam. John Springfield alifariki dunia Februari 21, mwaka 1891 na kuzikwa kwenye makaburi ya Stoughton Road, Guildford.
Miriam alizaa watoto wa kike wawili miaka ya 1896 na 1897 na mwaka 1899 alizaa mtoto wa kiume. Akiwa mjini Guildford, John Springfield alikuwa akifanyakazi ya kushona viatu, na kama nilivyosema hapo awali, alikuwa pia akifundisha ushonaji viatu. Huyu anakuwa Mzanzibari wa kwanza kuendesha kampeni dhidi ya utumwa na kule alikoishi.

1 comment: