Sunday 30 June 2013

Wafanyabiashara changamkia..Biashara na USA



Wafanyabiashara changamkia

 ujio wa Obama



Rais Barack Obama anawasili nchini kesho kwa ziara ya siku mbili. Pamoja na kufuatana na familia yake, Rais huyo pia ataongoza ujumbe wa watu zaidi ya 700 wengi wao wakiwa wafanyabiashara wakubwa wanaotafuta fursa za uwekezaji hapa nchini.
Hivyo, asijidanganye mtu kwamba Rais Obama na ujumbe wake wa wafanyabiashara wanakuja nchini kupiga siasa au kuimbiwa ngonjera na taarabu. Wala asijidanganye mtu kwamba Marekani imefanya madhumuni ya ziara hiyo kama siri kubwa ili nchi hiyo iweze kuwazuga na kuwahadaa viongozi wetu kwa lengo la kuchukua rasilimali zetu kirahisi.
Marekani tayari imeitangazia dunia na wananchi wa Marekani waliokuwa wakiikosoa ziara hiyo wakidai ingekuwa mzigo kwa walipa kodi wa nchi hiyo, kwamba ziara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Marekani na kwamba nchi hiyo ilifanya makosa makubwa kuiachia China kujitanua na kujiimarisha barani Afrika kwa kuingia mikataba ya kiuchumi na nchi mbalimbali. Ziara ya Rais Xi Jinping wa China nchini Tanzania hivi karibuni pia imeizindua Marekani kutoka usingizini, hivyo kaulimbiu ya Marekani hivi sasa ni ‘kutangulia sio kufika’.
Watanzania tunapaswa kuuona ujio wa Rais Obama na ujumbe wake katika muktadha huo. Ni ujio wa kibiashara na kiuchumi ambao Serikali na wafanyabiashara wetu wakijipanga vizuri na kutanguliza weledi na uzalendo nchi yetu nayo itafaidika na ziara hiyo. Katika mazungumzo na mapatano na ujumbe huo kabla ya kusaini mikataba, mkakati wetu kitaifa uwe ‘nipe nikupe’ na tusikubali hata kidogo kuingia tena mikataba ya ghiliba na ya ujanjaujanja.
Jambo muhimu hivi sasa ni kuwauliza wafanyabiashara na viongozi wa Serikali jinsi walivyojipanga kuingia katika mazungumzo na ujumbe huo. Tusijidanganye. Ujumbe wa Rais Obama utakuwa na wataalamu wa hali ya juu wa mapatano ya kibiashara za kimataifa (international trade negotiators).
Kwa kawaida, wengi wao huwa ni maprofesa waliobobea wa vyuo vikuu ambao wana nadharia na ujuzi mkubwa katika kile kinachoitwa mchezo wa mapatano (negotiation game). Hivyo, Wamarekani wataingia kwenye mapatano wakiwa tayari wanajua watoe nini na wachukue nini, kwa maana ya kutawala mchakato mzima na kujua ni wakati gani wasonge mbele au warudi nyuma.
Ni wazi kwamba itakuwa balaa kubwa kwa nchi yetu iwapo wawakilishi wetu wataingia katika mazungumzo hayo kichwakichwa. Tatizo tunaloliona hapa ni kwamba mazungumzo hayo yatahusu pia masuala yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu, yakiwamo uchimbaji wa gesi, mafuta, urani na madini. Sisi hatuna wataalamu wazalendo waliobobea katika nyanja hizo, hivyo tunaishauri Serikali isione haya kutafuta washauri mabingwa waelekezi ambao ni waaminifu na waadilifu ili washiriki katika mazungumzo hayo.
Huu sasa ni wakati mwafaka kwa nchi yetu kutumia ushindani wa kibiashara kati ya Marekani na China ili tunufaike. Serikali ijipange vizuri kuweka wazi sera za nchi kuhusu biashara ya nje na matumizi ya rasilimali zetu na itayarishe maeneo ambayo tayari imetenga kwa wawekezaji.
Ni matarajio yetu kwamba wafanyabiashara wetu katika sekta binafsi katika nyanja za utalii, biashara na viwanda nao watajipanga vyema kukutana na wenzao kutoka Marekani. Jambo wanalopaswa kuzingatia ni kwamba ujumbe wa Rais Obama unakuja nchini kutafuta fursa za kibiashara na kiuchumi na siyo vinginevyo.

No comments:

Post a Comment